Kwa mujibu wa ripoti ya kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Pedro Sánchez alisema: Serikali ya Uhispania inaendelea kufuatilia kwa karibu hali ya kulinda raia wake walioko kizuizini chini ya utawala wa Israel, lakini akasisitiza kuwa; hatua hiyo pekee haitoshi. Aliutaka Umoja wa Ulaya kusimamisha makubaliano ya ushirikiano na utawala huo, na pia kumtaka Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kuheshimu sheria za kimataifa za baharini.
Msafara wa kimataifa wa Samud uliandaa harakati iliyopewa jina la “Misheni ya Masika 2026”, ambapo meli hizo ziliondoka siku ya Jumapili kutoka kisiwa cha Sicily nchini Italia kwa lengo la kuvunja mzingiro usio wa kibinadamu wa Israel dhidi ya watu wa Ghaza na kufikisha misaada ya kibinadamu kwao.
Hata hivyo, kwa masikitiko, usiku wa Jumatano, boti zilizokuwa zikishiriki katika misheni hiyo zilishambuliwa na jeshi la Israel katika maji ya kimataifa karibu na pwani ya Crete. Jumla ya boti ishirini na moja zilikamatwa na utawala wa Kizayuni, huku boti 17 zikifanikiwa kufika katika maji ya ndani ya Ugiriki na nyingine 14 zikiendelea na safari zao.
Hii ni misheni ya hivi karibuni ya msafara huo kufuatia operesheni yao ya awali ya Septemba 2025, ambayo nayo ilikumbana na shambulio kama hilo mwezi Oktoba, ambapo utawala huo ulikiuka sheria za kibinadamu na kusababisha kukamatwa kwa mamia ya wanaharakati wa misaada ya kibinadamu.
Katika kipindi cha miaka miwili ya vita visivyo na uwiano dhidi ya wananchi wasio na ulinzi wa Ghaza, zaidi ya watu 72,000 wameuawa na zaidi ya Wapalestina 172,000 kujeruhiwa, pamoja na uharibifu mkubwa wa miundombinu, ikiwa ni pamoja na vituo vya afya katika eneo hilo.
Maoni yako